Ni pigo, jitimai na simanzi kubwa kwa Tanzania, jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika nzima kwa kifo chake Dr. Pombe Magufuli, rais mtukufu wa Tanzania. Marehemu alikuwa kiongozi shunjaa aliyejitenga kwa ubaladhuli, ufisadi na ukandamizaji wa viongozi wengi humu Afrika! Majonzi iliyoje!
Rais Dr. Magufuli atakumbukwa kama kiongozi halisi aliyefanya mabadiliko makubwa kama vile kuongoza kujenga na kuinua uchumi wa Tanzania, kupigana na uchochole na kutiribua magenge ya viongozi wafisadi.
Ni dhahiri kwamba marehemu alisimama kidete kupigania hali halisi na kuhakikisha kwamba hakuna mabilionea wa ufisadi wa furushi la COVID-19 Tanzania kama ilivyo hapa Kenya.
Magufuli pia alisimamia kwa imani kubwa na mapenzi ya walokole ambao aliwapigania kwa hali na mali na kuwainua kiuchumi na kimaisha. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu Magufuli.
Itakumbukwa kwamba wakati marais wa Afrika wakijitia hamnazo na kuabudu sera hafifu na za kiukoloni za mataifa yaliyoendelea, Rais Magufuli alisimama kidete na kwa umahiri na hekima kubwa kupingana na wenzake.
Ni dhahiri shahiri kwamba marehemu hakuwa mkaidi kama nchi za ughaibuni zaonekana kusimamia, rais Pombe alikuwa kiongozi stadi aliyetekeleza wajibu wake namna ilivyofaa. Wampende wampende, uongozi wake Ni wa kuigwa!
Kiongozi wa milenia tumempoteza kwa mwili ila sera na hekima aliyotuachia haitadidimia katu kwa kumbukumbu zetu. Hivyo, viongozi wa Afrika na kila mmoja wetu twafaa kuiga marehemu.
Walakini, mwenyewe na watu Wengi duniani twampenda marehemu ila Mungu kampenda zaidi. Tufanyeni ila kukubali japo kwa machozi? Mola amlaze Rais Mtukufu Magufuli mahali pema peponi.
🖋️Gitau wa Kung'u
No comments:
Post a Comment